Repayments

1.0 MUONGOZO WA UREJESHAJI MIKOPO

Sheria Namb. 3/2011 ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar kifungu cha 22(1) (b) kimeeleza wajibu wa kila mnufaika wa mkopo unaotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (BMEJZ) kurejesha mkopo huo Serikalini kupitia (BMEJZ) mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo au kabla ya hapo kadiri Bodi itakavyoona inafaa.

Kila mdaiwa ni lazima alipe deni lote analodaiwa na Bodi likijumuisha fedha alizolipwa mkononi/au kupitia akaunti yake ya benki na zilizolipwa moja kwa moja kupitia akaunti za Chuo alichosoma.

Mkopaji anaweza kurejesha mkopo wake wote kwa pamoja au kwa kiwango maalum cha malipo kwa mwezi ndani ya muda maalum uliowekwa na Bodi kulingana na kima cha mkopo aliopewa.

1.1      Wajibu wa Mkopaji

·       Kutoa taarifa kwa uongozi wa BMEJZ kuhusu kuhitimu masomo yake na kupata ajira.

·       Kutoa taarifa sahihi ziwemo anwani ya makazi, mwajiri au pahala pa kazi endapo mkopaji atakuwa ni mjasiriamali.

·       Kuanza marejesho ya mkopo kwa kumtaka mwajiri wake kukata deni analodaiwa na BMEJZ kutoka katika mshahara wake wa kila mwezi na kuwasilisha mikato hiyo ofisi za Bodi kwa utaratibu ambao Bodi itaona unafaa.

·       Mdaiwa ambaye si muajiriwa atalipa mkopo wake kwa kiwango maalum kwa mwezi ambacho atakubaliana na BMEJZ.

1.2 Adhabu kwa wanaokwepa kurejesha Mikopo Yao

Endapo mkopaji atashindwa kurejesha mkopo baada ya kufika kwa muda wa marejesho,

·       Atalazimika kulipa kiasi chote cha mkopo na gharama nyenginezo zinazoweza kutokea kutokana na kukwepa kulipa mkopo wake ikiwa ni pamoja na tozo ya mawakili.

·          Bodi inaweza kumfikisha kwenye vyombo vya sheria na kufungua mashtaka ya madai kwa mkopaji atakayekiuka wajibu wake wa kulipa deni analodaiwa na Bodi.

·          Kutozwa faini isiyopungua shilingi 50,000 kwa mwezi kwa kila marejesho ambayo hayatowasilishwa kwa wakati stahiki.

·          Bodi inaweza kuchukua hatua nyengine zozote, kwa mujibu wa sheria, itakazoona zinafaa dhidi ya mdaiwa.

1.3      Muda wa Marejesho

?  Mkopaji ambaye wakati wa kuomba mkopo hakuwa na ajira, anapaswa kuanza marejesho yake baada ya kumalizika kipindi cha mwaka mmoja cha msamaha (grace period) tokea kuhitimu masomo yake.

·          Mkopaji ambaye wakati wa kuomba mkopo alikuwa ni mwajiriwa au amejiajiri, anapaswa kuanza marejesho ya mkopo mara tu baada ya kuhitimu masomo yake au ndani ya muda wowote ambao Bodi itaona unafaa.

·          Mkopaji anapaswa kuendeleza mfululizo wa marejesho ya mkopo wake ndani ya muda uliowekwa na BMEJZ bila ya kusita kwa marejesho hata kwa mwezi mmoja. Hata hivyo Bodi inaweza kubadilisha muda wa mwisho wa marejesho kulingana na kiwango cha deni, uwezo wa kulipa wa mkopaji, utayari na uaminifu wa mkopaji kulipa deni lake, muda wa mkataba wa ajira uliobaki kabla ya kustaafu.

1.4    Rufaa kwa Wasiriodhika na Madeni yao

Mkopaji ambaye hatoridhika na deni lake atakalokabidhiwa na Bodi baada ya kuhitimu masomo yake anaweza kukata rufaa kwa kuomba kufanyika uhakiki mpya ya deni lake kwa utaratibu ambao Bodi itaona unafaa. Muombaji mwenye haki ya kukata rufaa na kusikilizwa ni yule ambaye:

a)     Ametoa taarifa kwa Bodi mara baada ya kuhitimu masomo yake.

b)    Amewasilisha rufaa yake kimaandishi akiambatisha na vielelezo vitakavyohitajika ndani ya siku 30 tokea tarehe aliyopokea barua ya kumjulisha deni lake na inayomtaka kuanza taratibu stahiki za kuanza marejesho ya mkopo wake.

c)     Barua yake ya rufaa inaonesha vipengele anavyodai vipitiwe upya na Bodi.

d)    Ameanza kurejesha deni lake wakati anasubiri kutolewa maamuzi ya rufaa yake.

1.5    Wajibu wa Mdhamini wa Mkopaji

Mdhamini wa mkopaji anawajibika:

·       Kutoa taarifa kwa Bodi kuhusu kumaliza masomo na/au kupata ajira kwa mkopaji.

·       Kutoa taarifa sahihi za mkopaji zikiwemo anwani ya makazi, mwajiri au pahala pa kazi endapo mkopaji atakuwa ni mjasiriamali.

·       Kumshajiisha mkopaji kulipa deni lake kwa wakati kwa utaratibu uliopangwa na Bodi.

·       Kulipa deni endapo mdaiwa atakwepa kulipa deni kwa hiari na kutotekeleza masharti ya marejesho ya mkopo. Aidha, mdhamini au mtu mwengine yeyote (wakala) anaweza kumlipia mkopaji deni lake kwa hiari.

1.6    Adhabu kwa Mdhamini anayekiuka wajibu wake

Mdhamini atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kama ifuatavyo:

·       Kutozwa faini inayofikia shilingi milioni 5 au kufungwa jela kwa kifungo kisichopungua miezi 12 au adhabu zote mbili kwa pamoja kwa kushirikiana na mdaiwa kukwepa kulipa deni analodaiwa. (Kifungu cha 27(2) cha Sheria ya Bodi).

·       Kulipa deni lote linalodaiwa pamoja na tozo nyenginezo ambazo Bodi itaona zinafaa kulipwa (Kifungu cha 27(3) cha Sheria ya Bodi). 

1.7    Wajibu wa Mwajiri

·       Kila mwajiri anapaswa kuijuilisha Bodi mtumishi mpya anayeajiriwa ndani ya miezi mitatu ili Bodi ijiridhishe kama mwajiriwa huyo ni mdaiwa wa Bodi au la.

·       Ikithibitika kuwa mwajiriwa ni mdaiwa wa Bodi, mwajiri atapaswa kukata kiwango cha deni kutoka kwenye mshahara wa kila mwezi wa mdaiwa kwa utaratibu ambao Bodi itaona unafaa.

·       Mwajiri atawajibika kuwasilisha mikato ya mshahara wa kila mwezi wa mdaiwa si zaidi ya siku 15 za mwezi unaofuata kwa utaratibu utakaotolewa na Bodi.

·       Kwa kukubali kumwajiri mdaiwa wa BMEJZ, mwajiri hatokuwa na nafasi ya kukwepa wajibu wake wa kuanza kukata mshahara wa mdaiwa na kuwasilisha marejesho kwa BMEJZ kwa kisingizio cha kutokuwa mshiriki katika mkataba wa mkopo kati ya BMEJZ na mdaiwa.

1.8    Adhabu kwa Mwajiri Anayekiuka Wajibu Wake

Mwajiri atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria zifuatazo:

·          Kutozwa faini au tozo nyengine yoyote ile ambayo Bodi itaona inafaa kwa kuchelewa kuwasilisha kwa wakati mikato ya mshahara wa mdaiwa kwenye ofisi za Bodi (Kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Bodi).

·          Kutozwa faini inayofikia shilingi milioni tano au kufungwa jela kwa kifungo kisichopungua miezi 12 au adhabu zote mbili kwa pamoja kwa kushindwa kukata deni la mdaiwa wa Bodi kutoka kwenye mshahara wake na kuwasilisha mikato hiyo kwenye ofisi za Bodi (Kifungu cha 27(2) cha Sheria ya Bodi).

·          Kulipa deni lote linalodaiwa pamoja na tozo nyenginezo ambazo Bodi itaona zinastahiki kulipwa (Kifungu cha 27(3) cha Sheria ya Bodi).