1.0
MAELEKEZO MUHIMU KWA WAOMBAJI WAPYA
Uongozi wa
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar unapenda kuwajulisha waombaji wote wa Mikopo
ya Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2021/22 kuwa maombi yao wanapaswa
kuyawasilisha kupita mfumo malum wa maombi ya mtandaoni unaojulikana ZHELB Online Loans Application System (ZOLAS).
Mtandao
huu umeunganishwa na mitandao ya Tasisisi nyengine za Elimu ya Juu, Fedha na
vitambulisho zikiwemo Tume ya Taifa ya Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Mafunzo ya
Ufundi (NACTE), Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na Mamlaka ya Usajli wa
Matukio Maalum ya Kijamii ya Zanzibar (ZCSRA) inayotoa vitambulisho vya
Mzanzibari Mkaazi. Mwombaji hatohitajika kujaza taarifa zinazopatikana katika
taasisi.
Aidha,
ZOLAS imeunganishwa na mfumo maalum wa malipo na ujumbe mfupi wa maneno (sms)
kupitia mitandao ya simu.
Waombaji wote
wanafahamishwa kuzingatia mambo yafuatayo:
i. Kuwa na kitambulisho
cha Mzanzibari.
ii. Kuhakikisha kuwa nambari
ya mtihani wa kidato cha nne iwe sawa na nambari aliyoituma kuwasilisha maombi
ya kujiunga na chuo.
iii. Kuhakikisha kuwa
majina yake matatu yanayotumika kwenye kitambulisho cha Mzanzibari na kidato
cha nne yanalingana.
iv.
Wahitimu wa nje ya Tanzania wawe na ithibati
ya ulinganisho (Equivalence) kutoka NECTA kwa kidato cha nne na sita, NACTE kwa
Stashahada na TCU kwa Shahada.
v.
Wahitimu wa Stashahada wawe na Award Verification Number (AVN) kutoka
NACTE).
vi. Kuwa na baruapepe (email) binafsi na ambayo haitobadilika kwa wakati
wote wa mchakato wa maombi.
vii. Kuwa na nambari ya
simu iliyosajiliwa.
viii.Kuhakikisha kufanya
malipo stahiki ya maombi kwenye akaunti ya BMEJZ baada ya kufungua akaunti na
kupatiwa nambari ya kumbukumbu (control number) ya kufanyia malipo hayo.
ix. Kurudufu (scanning)
nyaraka zote muhimu zinazohitajika wakati wa maombi zikiwemo barua za
kukubaliwa kujiunga na masomo, matokeo (transcript) na vyeti vya kumalizia
masomo kwa waombaji shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu. Waombaji wote wa
vyuo vya nje ya nchi mbali ya kuwa na barua za kujiunga na chuo wanapaswa pia
kuambatisha barua kutoka Tume ya Taifa ya Vyuo Vikuu zinazoridhia kujiunga na
Chuo na kusoma fani husika.
x. Maombi ya mikopo
yanapaswa kuwa na taarifa sahihi.
2.0
JINSI YA KUTUMA MAOMBI
Waombaji
watume maombi kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya BMEJZ (https://zhelb.go.tz) na kubonyeza
kitufe cha Online Loan Application System. Aidha, waombaji wanaweza kutuma
maombi yao kupitia kiunganishi zolas.zhelb.go.tz/zolas.
Ili
kuweza kuwasilisha maombi hayo, kila mwombaji anatakiwa kukamilisha hatua
zifuatazo:
2.1
Kujisajili
Baada
ya kubofya kiunganishi zolas.zhelb.go.tz/zolas utafunguka
ukarasa ambao mwombaji atapaswa kujaza nambari ya Kitambulisho cha Mzanzibar
Mkaazi na nambari ya mtihani wa kidato cha nne.
Angalizo:
· Majina
matatu ya muombaji yanayotumika kwenye kitambulisho cha Mzanzibari na kidato
cha nne yanalingana. Vyenginevyo utashindwa kusajiliwa na kuendelea na hatua
nyengine zinazofuata.
· Nambari
ya mtihani wa kidato cha nne iwe sawa na nambari iliyotumika kuwasilisha maombi
ya kujiunga na chuo
Baada
ya kukamilika kwa hatua hii, mwombaji ataingiza nambari yake ya simu ya
mkononi, anuani ya baruapepe na nambari ya mtihani wa kidato cha sita akiwa ni
mhitimu wa kidato cha sita au nambari maalum ya utambulisho (Award
Verfication Number – AVN) kwa mhitimu wa Stashahada.
2.2
Kufungua akaunti (ZHELB Online Student Account)
Baada
ya mwombaji kukamilisha kujisajili, mfumo wa ZOLAS utamtumia nambari maalum (Code)
kwenye anuani ya baruapepe aliyowasilisha. Mwombaji ataingia tena katika mfumo
wa ZOLAS na kufungua akaunti ambayo jina
la mtumiaji (username) itakuwa na
nambari yake ya Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na neno la siri (password)
atatumia nambari maalum aliyotumiwa. Baada ya kufungua akaunti, mwombaji
anapaswa kubadilisha nambari maalum aliyotumiwa kwa kuingiza neno jipya la siri
kulingana na chaguo lake.
2.3
Kutuma maombi
Ufunguzi
wa akaunti unamwezesha mwombaji kutuma maombi kwa kufuata maelekezo yaliyopo na
kujaza kikamilifu kila kipengele husika ikiwa ni pamoja na waombaji wa mikopo
kulipa TZS 20,000 ambazo ni gharama za
maombi zinazolipwa kupitia mitandao ya simu ya mkononi. Malipo yatafanyika
baada ya mwombaji kupatiwa nambari maalum (control number). Malipo
yatakayofanyika bila ya kutumia nambari maalum hayatozingatiwa.
Kwa maelezo
zaidi tembelea zolas.zhelb.go.tz/zolas.
3.0
SIFA ZA WAOMBAJI
3.1
SIFA ZA KUPATA MIKOPO
Sifa
za waombaji wa mikopo ambao maombi yao yanaweza kuzingatiwa wakati wa uteuzi
zimetajwa kwenye kifungu cha 20 cha Sheria Na. 3/2011 ya BMEJZ.
Sifa
hizo ni zifuatazo:
a) Awe
Mzanzibari mwenye kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.
b) Awe
amewasilisha maombi yake kupitia mfumo wa mtandao wa maombi wa BMEJZ ndani ya
muda maalum uliowekwa.
c) Awe
amepata alama nzuri za ufaulu zinazomruhusu kupata udahili kwenye chuo cha
elimu ya juu kinachotambuliwa na mamlaka husika nchini
i.
Mwombaji wa shahada ya kwanza (Bachelor/First
Degree) aliyehitimu kidato cha sita anapaswa awe amefaulu angalau
masomo mawili (Principal subjects) kwa alama za ufaulu zinazoanzia 4.0.
Mwombaji aliyehitimu Stashahada anatakiwa kuwa na alama za ufaulu (GPA)
zinazoanzia 3.0.
ii.
Mwombaji wa shahada ya uzamili (Master/Second
Degree) au shahada ya uzamivu (Doctor of Philosophy - PhD) awe na
ufaulu kuanzia daraja la pili.
iii.
Mwombaji mpya anayeendelea na masomo anaweza
kuomba kwa kuzingatia sifa za kitaaluma zilizotajwa hapo juu [c(i) –(ii)].
Aidha muombaji awe amefaulu mitihani yake ya chuo kwa kiwango kitakachomwezesha
kuendelea na masomo kwa mwaka unaofuatia katika ngazi ya masomo anayoombea
mkopo.
d) Awe
ameomba fani inayolingana na vipaumbele vya Taifa (Angalia Kiambatisho Na. 1).
e) Asiwe
na mkopo au udhamini wa masomo kutoka taasisi nyengine.
f) Ukomo
wa umri wakati wa kutuma maombi usiozidi miaka 35 kwa Mwombaji wa shahada ya
kwanza, miaka 45 kwa mwombaji wa shahada ya uzamili na miaka 47 kwa mwombaji wa
shahada ya uzamivu.
g) Mwombaji
anayedaiwa na BMEJZ awe ameshaanza kulipa deni lake kwa angalau asilimia 25 ya
deni lote bila ya kusita kwa malipo ya deni ya kila mwezi. Ikumbukwe kuwa
malipo ya asilimia 25 ya mkopo wa awali siyo dhamana ya kupangiwa mkopo.
h) Mwombaji
aliyesoma kwa mkopo kutoka BMEJZ awe ameshafanya kazi kwa angalau miaka miwili
baada ya kuhitimu masomo yake ya awali kabla ya kuomba mkopo mwengine kutoka
BMEJZ.
i) Waombaji
wa vyuo vya nje wapate ithibati ya kukubaliwa kujiunga na chuo (No
Objection Certificate) kutoka Tume ya Vyuo Vikuu ya Tanzania.
Wanafunzi
wanaoendelea na masomo ambao ni wanufaika wa mikopo hawahitajiki kuwasilisha
maombi mapya ya mikopo. Wanafunzi hao wanapaswa kujaza mikataba kwa kila mwaka
mpya wa masomo unapoanza pamoja na kuwasilisha matokeo ya mitihani.
4.0
UTEUZI WA WAOMBAJI
4.1
KUTANGAZWA WAJINA YA WAOMBAJI WALIOTEULIWA
Orodha za
majina ya waombaji walioteuliwa kwa kila chuo na fani yatatangazwa kupitia
tovuti za BMEJZ na WEMA katika mwezi wa Oktoba
2021. Aidha, kila mwombaji atakayeteuliwa atatumiwa taarifa ya uteuzi
kupitia baruapepe na ujumbe mfupi wa simu.
4.2
KUJAZA MIKATABA
Mkataba ni hati ya
makubaliano kati ya BMEJZ na mwanafunzi ambapo BMEJZ itampatia muombaji mafao
stahiki baada ya muombaji huyo kutimiza masharti yote yaliyoainishwa kwenye
Mkataba.
4.2.1 MIKATABA YA WAOMBAJI
WAPYA
Waombaji
wapya wa mikopo na ufadhili wa masomo wa SMZ watapaswa kujaza mikataba ili
kuweza kunufaika na mafao yanayotolewa na BMEJZ. Ili kuweza kujaza mkataba,
mwombaji aliyeteuliwa atapaswa kuingia kwenye akaunti yake aliyoitumia wakati
wa kuwasilisha maombi ya mikopo au ufadhili wa masomo wa SMZ.
Kupitia
akaunti hiyo, mwombaji atapatiwa nambari maalum ya kumbukumbu ya kufanya malipo
(Control
Number) kabla ya kuendelea na hatua nyengine za kujaza mikataba.
4.2.2 MIKATABA YA WANUFAIKA
WANAOENDELA NA MASOMO
Wanufaika
wa mikopo na ufadhili wa masomo wa SMZ wanaoendelea na masomo mwaka 2021/22
katika Taasisi mbalimbali za Elimu ya Juu za ndani na nje ya nchi ambao
hawakutuma maombi yao kwa njia ya mtandao, wataendelea kujaza mikataba inayopatikana
katika ofisi za BMEJZ za Unguja na Pemba.
Wanafunzi
waliojaza mikataba yao ya awali kwa njia ya mtandao, watapaswa kujaza mikataba
mipya kwa kuhuisha taarifa zao kulingana na mwaka wa masomo uliopo.
5.0
MAFAO KWA WAOMBAJI WA MIKOPO
5.1
VIPENGELE VYA MAFAO
Kwa kuzingatia uhitaji wa waombaji wa mikopo na ufadhili wa masomo wa
SMZ, BMEJZ
inalipa gharama za masomo kwa baadhi ya mafao kama ifuatavyo:
Na. |
Mafao kwa waombaji wa mikopo vyuo vya ndani |
Mafao kwa waombaji wa mikopo wa vyuo vya nje |
1. |
Ada ya masomo na mitihani |
Ada ya masomo na mitihani |
2. |
Posho la chakula na malazi |
Posho la chakula na malazi |
3. |
- |
Tiketi ya ndege |
4. |
- |
Bima ya afya |
5.2
UTARATIBU WA MALIPO
Posho la
chakula na malazi, gharama za vitabu na viandikwa na gharama za mafunzo kwa
vitendo zitalipwa moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya mwanafunzi. Ada ya
masomo na mitihani na mahitaji maalum ya kitivo yatalipwa moja kwa moja kwenye
Taasisi husika.
6.0
WAOMBAJI WA MIKOPO NJE YA NCHI
Kwa mwaka
2021/22, waombaji wa masomo katika Taasisi za Elimu ya Juu za nje ya nchi
watakaoteuliwa kupata mikopo ni wale amabao fani za masomo yao ni za Vipaumbele
vya Taifa na hazifundishwi katika Taasisi za Elimu ya Juu za Tanzania hasa
katika kada maalum za afya, uhandisi, mafuta na gesi, kilimo, uvuvi na tiba za
mifugo.
Waombaji
wapya wa mikopo wanaotarajia kujiunga au wanaoendelea na masomo katika taasisi
za elimu ya juu nje ya Tanzania, wanapaswa kuchagua ama kulipwa ada ya masomo
au posho la kujkimu pekee. Hakuna mwanafunzi atakayelipiwa ada ya masomo na
posho la kujikimu kwa pamoja.
Aidha,
malipo ya ada yamewekwa ukomo maalum unaolingana na US$ 3,200 kwa mwaka na tofauti ya ada itakayojitokeza italipwa na
mwafunzi husika. Utaratibu huu unatekelezwa ili kumjengea mnufaika wa mikopo ya
BMEJZ mazingira wezeshi ya kurejesha deni lake bila ya usumbufu baada ya
kuhitimu masomo yake.