Mikopo hutolewa kwa waombaji wa elimu ya juu waliotimiza sifa na vigezo kama vinavyoainishwa na kifungu cha 20 cha Sheria Namba 3/2011 na kifungu cha 3 cha Kanuni za Bodi. Kulingana na tafsiri iliyotolewa na Sheria ya Bodi, elimu ya juu ni ngazi ya elimu inayoanzia Shahada ya Kwanza (Bachelor/First Degree) au ngazi nyengine ya mafunzo inayolingana na shahada ya kwanza na kuendelea.

Elimu ya juu hutolewa na vyuo vikuu na vyuo vyengine vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi vinavyotambuliwa na mamlaka husika nchini zikiwemo Kamisheni ya Vyuo Vikuu (Tanzania Commission for Universities – TCU) na Baraza la Mafunzo ya Ufundi (The National Council for Technical Education - NACTE).

Mamlaka ya Utoaji Mikopo ya BMEJZ

Sheria Namba 3 ya 2011 inatoa mamlaka kwa BMEJZ ya kuongoza na kusimamia mchakato wa utoaji mikopo kwa waombaji kulingana na mahitaji na uwezo uliopo kwa wakati husika. Mamlaka ya Utoaji Mikopo ya BMEJZ ni pamoja na:

 • Kuamua vipengele vya mafao ya mkopo atakavyopatiwa muombaji;
 • Kuweka vigezo na sifa za msingi kwa muombaji wa mkopo;
 • Kuweka masharti maalum ya utoaji wa mikopo;
 • Kuamua idadi ya waombaji watakaopata mkopo kwa kila mwaka; na
 • Kusimamia fani za masomo kulingana na vipaumbele vya SMZ wakati wa utoaji wa mikopo.

Kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Bodi kinaitaka BMEJZ kutoa mkopo kwa kila muombaji, aliyetimiza vigezo na sifa za msingi za kupatiwa mkopo zilizowekwa na BMEJZ, ili aweze kulipa gharama zote au sehemu ya gharama za elimu ya juu kwa kipindi chote atachokuwa masomoni.

Maombi ya Kupatiwa Mkopo
Uchukuaji na Urejeshaji wa Fomu ya Maombi

Utaratibu wa utoaji wa mikopo hufanyika kwa wanafunzi wote wenye nia ya kupatiwa mikopo ya elimu ya juu kutuma maombi yao kwa kujaza Fomu Nambari 1 inayojulikana kama FOMU YA MAOMBI YA MKOPO WA MASOMO ambazo hutolewa na BMEJZ kama inavyoelekezwa na Kifungu cha 4 cha Kanuni za BMEJZ.

Kwa kawaida uchukuaji wa fomu za maombi ya mikopo huanza Mei 2 na kukamilika Julai 31 ya kila mwaka. Muda wa kuchukua na kurejesha fomu za maombi huweza kubadilika kadiri BMEJZ itakavyoona inafaa. BMEJZ hutoa matangazo kupitia njia mbalimbali za mawasiliano zikiwemo redio, vituo vya televisheni na tovuti za BMEJZ na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) ili kuwafikia watu wengi kadiri iwezekanavyo.

Fomu za maombi ya mikopo hutolewa kwa malipo kwa kiwango ambacho BMEJZ inaona kinafaa katika mwaka husika kwa kuzingatia gharama za uchapishaji, usimamizi wa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ya maombi na uwezo wa waombaji.

Fomu Nambari 1 ndiyo nyaraka ya msingi inayotoa mwelekeo wa muombaji kukubaliwa au kukataliwa maombi yake ya mkopo. Muombaji wa mkopo lazima ahakikishe kuwa ametimiza sifa za msingi za kuomba mkopo kama zilivyoanishwa hapo chini, amekamilisha kujaza taarifa zote zinazohitajika kwenye fomu na kuwasilisha viambatisho husika.

Utaratibu wote wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za maombi pamoja na taarifa za waombaji waliorejesha fomu hizo hufanyika kwa kuweka kumbukumbu za waombaji kwenye mfumo wa kompyuta (database) wa BMEJZ ulioandaliwa maalum kwa kazi hiyo. Katika hatua hii, taarifa za waombaji zinazoingizwa zinajumuisha tarehe ya uchukuaji wa fomu ya maombi, jina na jinsi ya muombaji, ngazi ya elimu ya juu aliyofikia, ngazi na fani ya elimu inayoombwa na tarehe ya urejeshaji wa fomu husika.

Fomu ya maombi itakayowasilishwa ikiwa na mapungufu au kurejeshwa baada ya kupitia muda wa mwisho wa urejeshaji haitopokelewa na watendaji wa BMEJZ na hivyo muombaji kupoteza nafasi ya kuweza kuzingatiwa kwa maombi yake ya mkopo wa masomo. Waombaji wa mikopo wanashauriwa kufuata maelekezo watakayopatiwa na watendaji wa BMEJZ wakati wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za maombi.

Mipango ya baadaye ya BMEJZ ni kuwa maombi yote ya mikopo yatafanyika kwa waombaji wenyewe kujaza taarifa zote kwenye mtandao (online application) na baada ya kukamilika kwa utiaji wa taarifa husika, muombaji atatakiwa kuichapa fomu hiyo na kuiwasilisha pamoja na viambatisho stahiki, vilivyothibitishwa na mahakama au wakili wa kujitegemea, kwenye ofisi za BMEJZ kwa uhakiki.

Muundo wa Fomu ya Maombi ya Mkopo

Fomu Nambari 1 imetayarishwa katika lugha nyepesi na utaratibu unaomuwezesha muombaji kujaza taarifa zake kwa urahisi. Mbali ya Utangulizi na Hitimisho, Fomu Nambari 1 imegawika katika sehemu kuu tatu. Nazo ni: Sehemu ya Kwanza; Sehemu ya Pili na Sehemu ya Tatu.

Utangulizi

Kwenye utangulizi, muombaji hutakiwa kujaza taarifa zifuatazo:

 • Nambari ya kitambulisho cha Mzanzibari na kitambulisho cha Taifa (Mtanzania) na kuambatanisha vivuli vya kitambulisho chake cha Mzanzibari na Mtanzania.
 • Nambari ya kituo, nambari ya mtihani na mwaka aliofanya mtihani wa mwanzo wa kidato cha nne
Sehemu ya Kwanza

Katika sehemu hii, muombaji anapaswa kujaza taarifa zake binafsi zikijumuisha;

 • Jina lake Kamili (kama linavyosomeka kwenye cheti chake cha kuzaliwa, vyeti vya masomo na vitambulisho);
 • Jinsi yake (mwanamume au mwanamke);
 • Tarehe ya kuzaliwa;
 • Nambari ya simu; na
 • Anwani ya makazi (ikiwemo namba ya nyumba, mtaa na shehia anayoishi).
Sehemu ya Pili

Katika sehemu hii, muombaji lazima ajaze sifa zake za kitaaluma zikiwemo:

 • Elimu yake ya msingi
 • Sifa za kitaaluma kuanzia kidato cha nne hadi ngazi ya mwisho ya elimu aliyofikia kabla ya kuomba ngazi nyengine ya elimu akionesha skuli au chuo alichosoma; masomo/fani aliyosoma, alama/madaraja ya ufaulu kwa kila somo na mwaka aliohitimu masomo yake.
 • Ngazi ya masomo, fani ya masomo anayoomba na chuo anachoomba udahili. Ni muhimu muombaji kuzingatia kuwa ngazi ya masomo anayoiombea mkopo isiwe ambayo aliwahi kudahiliwa katika chuo chochote na kutunukiwa cheti. Aidha masomo anayoomba kusoma yawiane na Vipaumbele vya SMZ kwa mwaka husika. Vilevile muombaji ahakikishe chuo cha ndani au nje ya nchi anachoomba udahili lazima kiwe kinatambuliwa na Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU) au Baraza la Mafunzo ya Ufundi (NACTE).
 • Mafao ya mkopo ambayo angependa kupatiwa pindipo atateuliwa kuwa miongoni mwa waombaji watakaopatiwa mikopo katika mwaka husika. Ni vyema kuzingatiwa kuwa BMEJZ haitolazimika kutoa mkopo kwa mafao ya mkopo yatakayoainishwa na muombaji. Utoaji wa mikopo unakwenda sambamba na uwezo wa BMEJZ katika mwaka husika. Hivyo BMEJZ haitowajibishwa kwa kutoa au kutokutoa kwa muombaji aina zote au mojawapo ya mkopo ulioombwa. Waombaji wa mikopo waliopata udahili katika vyuo vya nje ya Tanzania wanashauriwa kuainisha aina moja tu ya mafao ya mkopo kwa sababu BMEJZ inatoa mkopo kwa aina moja tu ya mafao kwa wanafunzi wa vyuo vya nje.
 • Mahitaji maalum ya vifaa vya kujifunzia kutokana na aina ya ulemavu aliyonayo muombaji mkopo. Walengwa wakuu ni walemavu wasioona au wenye uoni hafifu, viziwi na walemavu wa viungo. Mkopo utakaotolewa hautohusu vifaa kama vile viti vya magurudumu (wheel chairs), fimbo nyeupe (white cane), magongo ya kutembelea (stretchers) na kompyuta.
Sehemu ya Tatu

Sehemu hii hujazwa na waombaji walioajiriwa kwenye taasisi za umma au binafsi kwa kukamilisha taarifa zifuatazo:

 • Muombaji aliyeajiriwa lazima ataje jina na anwani ya Taasisi anayofanyia kazi, Kitengo/Kituo alichopangiwa kufanya kazi, nambari ya mshahara na nambari ya kadi ya uanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.
 • Mkuu wake wa kazi katika Taasisi husika mwenye mamlaka ya kutoa ruhusa za masomo athibitishe kumruhusu au kutomruhusu mwajiriwa wake kwenda masomoni katika ngazi na fani aliyoomba kwa mwaka anaouombea mkopo kutoka BMEJZ. Mkuu wa kazi atakayeidhinisha ruhusa ya kwenda masomoni kwa mhusika analazimika kutaja jina lake, wadhifa wake, kutia saini yake na kugonga muhuri wa taasisi. Ni vyema muombaji ahakikishe kuwemo kwenye mpango wa mafunzo wa Taasisi yake kabla ya kutuma maombi ya mkopo kwa BMEJZ ili kuepuka usumbufu wa kukosa ruhusa ya kwenda masomoni.

Kuanzia mwaka wa masomo 2017/18 waombaji wa mikopo walioajiriwa hawatozingatiwa isipokuwa kwa waombaji wa fani maalum za udaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu katika shahada za uzamivu (PhD) tu.

Hitimisho

Hitimisho la Fomu Nambari 1 linajumuisha uwepo kwa viambatisho vya muombaji kwa taarifa alizojaza kwenye Fomu pamoja na Kiapo cha Muombaji.

Viambatisho vinavyopaswa kuwasilishwa pamoja na Fomu Nambari 1 wakati wa kutuma maombi ya mkopo ni vifuatavyo:

 • Kivuli cha cheti chake cha kuzaliwa;
 • Vivuli vya vyeti vyake vya masomo kuanzia kidato cha nne hadi ngazi ya mwisho ya masomo aliyofikia;
 • Vivuli vya matokeo ya mitihani (transcripts) kwa ngazi zote alizozianisha kwenye fomu ya maombi;
 • Vivuli vya vitambulisho vya Mzanzibari na Mtanzania;
 • Kivuli cha barua ya udahili wa chuo kinachotambulika. Pindipo muombaji atakuwa mpaka wakati wa kutuma maombi hajapata barua ya udahili kutoka chuo alichoomba kujiunga nacho, fomu yake ya maombi itapokelewa na atapaswa kuiwasilisha barua ya udahili mapema iwezekanavyo kabla ya kutangazwa kwa majina ya waombaji walioteuliwa kupata mikopo;
 • Waajiriwa wawasilishe kivuli cha kitambulisho cha uanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya jamii na ithibati ya malipo ya mshahara (monthly salary slip) wa kila mwezi;
 • Waombaji wenye ulemavu wawasilishe kadi ya uanachama wa Jumuiya ya Ulemavu husika au uthibitisho kutoka taasisi inayotambulika inayosimamia maslahi na haki za watu wenye Ulemavu.

Vivuli vya viambatisho vyote lazima viwasilishwe baada ya kuthibitishwa na mahakama au wakili wa kujitegemea.

Kwenye Kiapo cha Muombaji, muombaji anatakiwa kuthibitisha usahihi wa taarifa alizojaza na viambatisho alivyowasilisha na kuwa tayari kurejesha mkopo atakaopatiwa mara baada ya kuhitimu masomo yake kwa kufuata utaratibu uliowekwa na BMEJZ.

Uteuzi wa Waombaji Watakaopatiwa Mikopo

Fomu za maombi zilizokamilika na kuwasilishwa kwa wakati huchambuliwa kwa kina na taarifa za muombaji zilizojazwa kwenye Fomu Nambari 1 huhamishwa na kuingizwa kwenye database ya BMEJZ ambapo kila muombaji hufunguliwa akaunti yake na kupewa utambulisho wa pekee. Ili kurahisisha uingizaji wa taarifa hizo, kila muombaji anapaswa kuhakikisha kuwa taarifa atakazotoa na viambatisho atakavyowasilisha ni sahihi. Tahadhari kubwa huchukuliwa wakati wa uingizaji wa taarifa za waombaji kwenye mfumo wa kompyuta ili taarifa zinazoingizwa ziwiane na taarifa zilizomo kwenye Fomu Nambari 1.

Taarifa zilizoingizwa kwenye mfumo wa kompyuta hutumika kutoa mapendekezo ya awali ya uteuzi wa waombaji wa mikopo ambao wametimiza sifa za msingi za uteuzi kwa mwaka husika. Orodha ya waombaji kwa kila ngazi ya masomo inayoombwa kulingana na uzito wa sifa za kila muombaji na fani iliyoombwa hutayarishwa kwa ajili ya uteuzi.

Vigezo vinavyotumika kutoa mapendekezo ya awali ya uteuzi wa waombaji watakaopatiwa mikopo unafuata utaratibu uliowekwa na vifungu vya 19 na 20 vya Sheria Namba 3/2011 ya BMEJZ na kufafanuliwa na vifungu vya 3 hadi 5 vya Kanuni za BMEJZ. Kwa ujumla vigezo vinavyotumika kutoa mapendekezo ya uteuzi ni kama vifuatavyo:

 • Alama za ufaulu za waombaji.
 • Kuwepo kwa ithibati ya mwanafunzi kukubaliwa kujiunga na chuo husika kabla ya uteuzi.
 • Fani inayoombwa kulingana na vipaumbele vya SMZ.
 • Umri wa muombaji.
 • Uwiano wa idadi ya waombaji katika fani mbalimbali.
 • Uwiano wa idadi ya waombaji wanaume na wanawake wanaopendekezwa kupatiwa mikopo.
 • Uwezo wa fedha wa BMEJZ kutoa mikopo kwa waombaji katika mwaka husika.
 • Uwepo wa waombaji waliopatiwa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya Jamhuri ya Muungano au Taasisi na Asasi nyengine zinazotoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria Namba 3/2011 na kifungu cha 8 cha Kanuni za BMEJZ, mapendekezo ya uteuzi wa majina ya waombaji wa mikopo yanatakiwa kuwasilishwa kwenye Kamati ya Elimu ya Juu inayoundwa na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa BMEJZ. Kazi ya Kamati ya Elimu ya Juu ni kuhakiki, kujadili na kupitisha majina ya waombaji walioteuliwa kupatiwa mikopo katika mwaka husika kwa kuzingatia vigezo vilivyotajwa hapo juu au vyenginevyo kwa kadiri Kamati ya Elimu ya Juu itakavyoona inafaa kwa wakati husika.

Hata hivyo, Kamati ya Elimu ya Juu imekasimu madaraka yake kwa Kamati ya Uteuzi ambayo uwepo wake umetimiza matakwa ya kisheria kama ilivyotajwa katika kifungu cha 14(5) cha Sheria ya BMEJZ. Kamati ya Uteuzi inaundwa na wajumbe watano wasiokuwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya BMEJZ. Wajumbe wa Kamati ya Uteuzi wanateuliwa na Mhe. Waziri anayesimamia shughuli za Elimu.

Wajumbe hao watatoka:

 • Tume ya Mipango ya SMZ.
 • Wizara inayosimamia Elimu.
 • Wizara inayosimamia Utumishi wa Umma.
 • Sekta binafsi.
 • Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (BMEJZ), ambayo itawakilishwa na Meneja Mikopo atakayekuwa pia Katibu wa Kamati ya Uteuzi.

Baada ya kumaliza kazi ya uteuzi wa waombaji wa mikopo ya elimu ya juu, Mwenyekiti ya kamati ya Uteuzi atakabidhi taarifa ya uteuzi’ pamoja na orodha za majina ya waombaji wanaopendekezwa kupatiwa mikopo, kwa mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Juu ambaye ataiwakilisha katika Kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa BMEJZ kwa ajili ya kuridhiwa na kutoa idhini ya kutangazwa kwa waombaji wote waliopatiwa mikopo.

Majina ya waombaji walioteuliwa kupatiwa mikopo hutangazwa kupitia tovuti ya BMEJZ (www.zhelb.go.tz), tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo wa Amali (www.moez.go.tz) au njia nyengine yoyote ambayo BMEJZ itaona inafaa na inayoweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa urahisi.

Idadi ya Waombaji Wanaoteuliwa Kupatiwa Mikopo

Hakuna idadi maalum iliyowekwa ya waombaji wanaoteuliwa kupatiwa mikopo kwa mwaka husika katika ngazi mbalimbali za masomo. Idadi ya wanaoteuliwa inategemea upatikanaji wa fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya waombaji wapya wa mikopo na idadi ya wanafunzi wanaoendelea na masomo yao vyuoni kupitia mikopo wanayopatiwa na BMEJZ.

Wakati wa uteuzi kipaumbele hutolewa kwa waombaji wanaotoka kwenye familia zenye kipato kidogo; wanawake na walemavu au wazazi wa muombaji wote ni walemavu au wenye maradhi ya kudumu na kuthibitishwa na daktari anayetambulika kuhusiana na kutokumudu kwao kujiingizia kipato cha kuweza kumlipia gharama za masomo mtoto wao.

Hivyo waombaji wenye uwezo wa kujilipia gharama za masomo au wanaotoka kwenye familia zenye uwezo wa kulipa gharama za masomo wanashauriwa kutokuomba mikopo kutoka BMEJZ ili kutoa nafasi kwa waombaji wasiojiweza kutumia nafasi chache za mikopo zilizopo.

Sifa za Kupata Mkopo

Sifa za waombaji wa mikopo ambao maombi yao yanaweza kuzingatiwa wakati wa uteuzi zimetajwa kwenye kifungu cha 20 zikiwemo:

 • Muombaji awe Mzanzibari
 • Awe ameomba mkopo kwa kujaza Fomu Nambari 1 au kupitia njia nyengine yoyote ile ambayo BMEJZ itaona inafaa. Maombi yawe yamewasilishwa ndani ya muda maalum uliowekwa na BMEJZ unaoanzia Mei 2 hadi Julai 31 ya kila mwaka.
 • Awe amepata udahili kwenye chuo cha elimu ya juu kinachotambuliwa na mamlaka husika nchini.
 • Awe amepata alama nzuri za ufaulu.
  • Muombaji wa shahada ya kwanza (Bachelor/First Degree) aliyehitimu kidato cha sita anapaswa awe amefaulu angalau masomo mawili ya mlinganisho (Principal subjects) kwa alama za ufaulu zinazoanzia alama (points) 4.0.
  • Muombaji wa shahada ya kwanza aliyehitimu stashahada ya kawaida (Ordinary Diploma) anatakiwa awe na ufaulu unaoanzia alama (GPA) 3.0 au B. Wahitimu wa “Full Technician Certificate (FTC)” wawe na ufaulu unaoanzia alama C.
  • Muombaji wa shahada ya uzamili (Master/Second Degree) katika masomo ya sanaa au sayansi jamii awe amehitimu shahada ya kwanza na kupata alama za ufaulu kuanzia daraja la pili la juu (upper second class). Waombaji wa shahada ya uzamili katika masomo ya sayansi, ufundi, tiba, uchumi, mipango na biashara wawe na alama za ufaulu za kuanzia daraja la pili la chini (lower second class). Wahitimu wa stashahada ya uzamili(Postgraduate Diploma) wanapaswa kupata alama za ufaulu kuanzia daraja la pili la chini (lower second class)
  • Muombaji wa shahada ya uzamivu (Doctor of Philosophy - PhD) awe amehitimu shahada ya uzamili na kupata alama za kuanzia daraja la pili la juu kwa waombaji wa masomo ya sanaa na sayansi jamii. Waombaji wa shahada ya uzamivu katika masomo ya sayansi, ufundi, udaktari na uchumi, mipango na takwimu wapate alama za ufaulu kuanzia daraja la pili la chini.
  • Waombaji wanaoendelea na masomo vyuoni pia wanaweza kuomba kwa kuzingatia sifa za kitaaluma zilizotajwa hapo juu [d(i) –(iv)]. Aidha muombaji awe amefaulu mitihani yake ya chuo kwa kiwango kitakachomwezesha kuendelea na masomo kwa mwaka unaofuatia katika ngazi ya masomo anayoombea mkopo.
  • Angalizo:
   Bodi inaweza kupitia upya sifa za kitaaluma kwa waombaji wa mikopo kulingana na mahitaji ya wakati husika
 • Awe ameomba fani inayolingana na vipaumbele vya SMZ katika mwaka husika.
 • Asiwe na mkopo au udhamini wa masomo kutoka taasisi nyengine.
 • Muombaji wa shahada ya kwanza asizidi umri wa miaka 35 wakati wa kuanza masomo na muombaji wa shahada ya uzamili asizidi miaka 40. Ukomo wa umri wa muombaji wa shahada ya uzamivu ni miaka 45 wakati wa kuanza masomo.
 • Muombaji aliyeajiriwa kwenye utumishi wa umma awasilishe barua ya ruhusa kutoka kwa mwajiri wake.
 • Muombaji anayedaiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar awe ameshaanza kulipa deni lake kwa angalau asilimia 25 ya deni lote bila ya kusita kwa malipo ya deni ya kila mwezi.
 • Muombaji aliyesoma kwa mkopo kutoka BMEJZ awe ameshafanya kazi kwa angalau miaka miwili baada ya kuhitimu masomo yake ya awali kabla ya kuomba mkopo mwengine kutoka BMEJZ.
 • Angalizo:
  • Waombaji wanaotumia sifa za masomo ya kidato cha nne kuomba udahili katika vyuo vikuu vya ndani au nje ya nchi ili kujiunga na masomo ya Shahada ya Kwanza, maombi yao ya mkopo hayatozingatiwa. Mfumo wa elimu wa Tanzania unaotumika kwa wakati huu unatambua sifa ya msingi kwa wahitimu wa elimu ya sekondari wanaodahiliwa kwa masomo ya Shahada ya Kwanza au ngazi inayolingana nayo katika vyuo vikuu na vyuo vyengine vya elimu ya juu ni kuhitimu masomo ya kidato cha sita.
  • Vilevile, waombaji wa mikopo waliohitimu masomo ya Diploma pasi na kuwa na elimu ya kidato cha sita au sifa za kujiunga na kidato cha sita, wanatakiwa wawe wamefaulu angalau masomo matano ya kidato cha nne kwa kiwango cha alama D na kuhitimu ngazi ya cheti (Certificate) kabla ya kujiunga na masomo ya Diploma (NTA 6).
Mafao ya Mikopo

Mafao ya mkopo ambayo BMEJZ inaweza kutoa kwa muombaji yameanishiwa kwenye Kifungu cha 19(2) cha Sheria Namba 3/2011. BMEJZ inaweza kutoa kwa ukamilifu au sehemu ya mafao ya mkopo yaliyoainishwa ambayo yanajumuisha:

 • Ada ya masomo
 • Ada ya mitihani
 • Posho la chakula na makazi
 • Gharama za vitabu na vifaa vyenginevyo vya kujifunzia
 • Nauli (inayoweza kulipwa ama mwanzo na mwisho wa kila mwaka wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo vya ndani; au kulipwa mwanzo wakati muombaji anakwenda chuoni kuanza masomo na baada ya kuhitimu masomo ya mwaka husika kwa vyuo vya nje.)
 • Posho la utafiti na/au kazi za vitendo
 • Gharama kwa ajili ya mahitaji maalum ya vitivo
 • Bima ya afya

Hata hivyo, Bodi imepewa mamlaka ya kisheria ya kuamua vipengele vya mafao ya mkopo atakavyopatiwa mwanafunzi husika na vipengele vitavyobakia vichangiwe na mwanafunzi mwenyewe, mzazi au mlezi wa mwanafunzi husika.

Masharti ya Mikopo
 • Kila muombaji atakayeteuliwa kupata mkopo awe tayari kujaza mkataba wa mkopo (Fomu Nambari 2) unaotolewa na BMEJZ na kukamilisha taarifa zote pamoja na kufuata masharti yote yaliyoainishwa kwenye mkataba. Mkataba huu unapaswa kujazwa mwanzo wa mwaka wa masomo kwa wanafunzi wapya na kurejea kujaza mkataba mpya kila mwanzo wa mwaka mpya wa masomo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenye ngazi ya masomo waliyokubaliwa kupatiwa mkopo na BMEJZ.
 • Malipo ya ada ya masomo, ada ya mitihani na gharama nyengine zinazopaswa kulipwa moja kwa moja kwa chuo zitalipwa kupitia akaunti ya chuo husika au njia nyengine ambayo BMEJZ itaona inafaa. Mtiririko wa malipo ya ada ya masomo utalingana na muda wa masomo wa ngazi husika kama utakavyoelezwa kwenye barua ya udahili.
 • Posho zinazopaswa kulipwa moja kwa moja kwa mwanafunzi, BMEJZ italipa kupitia akaunti itakayofunguliwa na mwanafunzi kwa maelekezo ya BMEJZ au njia nyengine ambayo BMEJZ itakayoona inafaa. Malipo ya posho yatalipwa kulingana na vigezo na uwezo wa Bodi. Kwa wanafunzi wa vyuo vya nje, malipo ya posho yatafanyika kulingana na kiwango cha ubadilishaji fedha za kigeni kilichotumika wakati wa kupitishwa kwa bajeti.
 • Malipo ya mkopo yatatolewa kwa utaratibu wa awamu au mkupuo kulingana na mfumo wa masomo katika Chuo husika au BMEJZ itakavyoona inafaa kulingana na uwezo wake.
 • Kiwango cha mkopo utakaotolewa kitakuwa na ukomo wa mwisho wa malipo (ceiling) wa gharama za masomo kwenye ngazi husika katika mwaka husika wa masomo. Mwanafunzi husika atawajibika kujilipia gharama za ziada. Ukomo wa mwisho wa malipo kwa mwaka wa masomo kwa wakopaji wa shahada ya kwanza ni shilingi 6,000,000/=; wakopaji wa shahada za uzamili shilingi 8,000,000/= na shahada za uzamivu ni shilingi 10,000,000/=.
 • Wakopaji waliodahiliwa kwenye fani zinazosomeshwa na vyuo vya ndani ya nchi kwa kushirikiana na vyuo vya nje ya nchi ambapo ada ya masomo hutozwa kwa shilingi ya Tanzania kwa ajili ya chuo cha ndani na fedha za kigeni kwa ajili ya chuo cha nje na kulipwa katika akaunti tofauti, BMEJZ italipa ada inayotozwa kwa shilingi za Kitanzania pekee. Sehemu ya ada inayotozwa kwa fedha za kigeni italipwa na mwanafunzi husika.
 • Wakopaji waliojiunga/wanaojiunga na vyuo vya nje kusoma fani adimu na zilizo kwenye vipaumbele vya SMZ watapatiwa aina moja ya mafao ya mkopo kulingana na chaguo lake au kwa njia yoyote ile ambayo BMEJZ itaona inafaa. Utaratibu huu umewekwa ili kuiwezesha BMEJZ kutoa mikopo inayorejesheka na kuongeza idadi ya waombaji wanaopatiwa mikopo.
 • Muombaji atakayerejea mwaka wa masomo katika ngazi husika, atapatiwa ruhusa ya kuendelea kupatiwa mkopo kwa mwaka mmoja wa ziada kulingana na muda wa masomo wa ngazi husika.
 • Muombaji ataruhusiwa kuahirisha masomo na kurejea masomoni mwaka unaofuata mara moja tu katika muda wote wa masomo katika ngazi ya masomo anayopatiwa mkopo. Mkopaji atakayeshindwa kurejea masomoni mwaka unaofuata baada ya kuahirisha, mkopo wake utasitishwa na kutakiwa kuanza marejesho ya mkopo.
 • Muombaji aliyeajiriwa asiwe na madeni kutoka taasisi nyengine yanayofikia zaidi ya theluthi moja ya mshahara wake kabla na hadi atakapomaliza mkataba wake wa mkopo na Bodi.
Mkataba wa Mkopo
 • Kifungu cha 11(b) cha Kanuni za BMEJZ kinamtaka kila muombaji aliyeteuliwa kupewa mkopo kujaza Mkataba wa Mkopo (Fomu Nambari 2) unaotayarishwa na BMEJZ.
 • Mkataba wa Mkopo ni hati ya makubaliano kati ya BMEJZ na mkopaji ambapo BMEJZ inapaswa kumpatia muombaji aina zote za mkopo alizoahidiwa kupatiwa kulingana na makubaliano baada ya muombaji huyo kutimiza masharti yote yaliyoainishwa kwenye Mkataba.
Muundo wa Mkataba wa Mkopo

Mkataba wa mkopo wa masomo kwa waombaji wapya umegawika katika sehemu kuu tano.

Sehemu ya kwanza: Wahusika wa Mkataba

Sehemu hii inawataja wahusika wakuu wa mkataba wa mkopo ambao ni BMEJZ (kwa upande mmoja) na Mkopaji ambaye ni mwanafunzi aliyeteuliwa kupewa mkopo (kwa upande wa pili). Katika sehemu hii mkopaji anatakiwa kueleza utambulisho wake kwa kutaja majina yake matatu (ambayo yawe sawa na majina aliyotumia kwenye cheti chake cha kuzaliwa na vyeti vya masomo); anwani yake ya posta na makazi; nambari ya mtihani, kituo cha mtihani na mwaka aliofanya mtihani wa kidato cha nne. Mkopaji anapaswa kubandika picha ya rangi inayoonesha vyema sura yake na iliyopigwa si zaidi ya miezi sita iliyopita.

Sehemu ya Pili: Masharti ya Mkataba

Sehemu hii imeorodheshwa masharti na wajibu wa kila mhusika wa mkataba wakati wa kutekeleza masharti ya mkataba. Aidha, sehemu hii inaeleza hatua zitakazochukuliwa na BMEJZ dhidi ya mkopaji pindipo atashindwa kutekeleza kikamilifu masharti ya mkataba.

Sehemu ya Tatu: Tamko la Mkopaji (Declaration)

Kwenye sehemu hii mkopaji anatakiwa kutoa tamko la kuthibitisha usahihi wa taarifa zake za kitaaluma na makazi atakazojaza kwa kuweka saini yake na kushuhudiwa na Hakimu au wakili wa kujitegemea. Taarifa za makazi zinajumuisha jina la mtaa, shehia na nambari ya nyumba Taarifa za kitaaluma zinazopaswa kujazwa ni pamoja na Chuo ambacho mkopaji amepata udahili; nambari ya usajili ya mwanafunzi; mwaka wa masomo aliopo chuoni; ngazi na fani ya masomo anayosoma; mwaka alioanza na anaotarajia kumaliza masomo.

Sehemu ya Nne: Ushuhuda wa Sheha

Sheha wa shehia husika anapaswa kuthibitisha taarifa za makazi za mkopaji kwa kuwepo muhuri wa Sheha. Ili kurahisisha mawasiliano, Sheha husika anapaswa kuandika jina lake na nambari yake ya simu.

Sehemu ya Tano: Wadhamini wa Mkopaji

Kila mwanafunzi anayepatiwa mkopo anapaswa kuwa na wadhamini wawili ambao:

 • Hawadaiwi na BMEJZ.
 • Ni wazazi, walezi au jamaa wa karibu wa mkopaji ambao wametimiza masharti ya kisheria ya kuweza kuwa wadhamini.
 • Watamdhamini mkopaji hadi kuhitimu masomo yake kwa ngazi ya masomo aliyoiombea mkopo. Endapo mmoja wapo wa wadhamini au wadhamini wote watajitoa kwenye udhamini, wadhamini hao watapaswa kutoa taarifa ya maandishi ya kujitoa kwao au mkopaji atatoa taarifa kwa uongozi wa BMEJZ za kujitoa kwa wadhamini hao na sababu za kujitoa kwao.
 • Ni Wazanzibari na wenye makaazi ya kudumu kwenye visiwa vya Zanzibar.
 • Mdhamini awe na umri usiozidi miaka hamsini wakati wa kuchukuwa dhaman kwa mara ya kwanza .
 • Kila mdhamini atawasilisha kivuli cha kitambulisho cha kazi au uwanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, kivuli cha kitambulisho cha Mzanzibari na kivuli cha kitambulisho cha Mtanzania.
 • Kila mdhamini atawasilisha barua yenye saini yake kuthibitisha kukubali kumdhamini mkopaji na kutekeleza masharti yote ya mkataba yakiwemo:
  • Kutoa taarifa kumhusu mkopaji kila wakati atakapotakiwa kufanya hivyo na BMEJZ.
  • Kuhakikisha kuwa mkopaji anaanza kurejesha deni lake baada ya kuhitimu masomo yake.
  • Kulipa deni lote endapo mkopaji atakwepa kutimiza wajibu wake wa kulipa deni lake kwa mujibu wa taratibu za BMEJZ.
  • Kutoa taarifa iwapo mkopaji atafariki, amepata maradhi ya kudumu, ulemavu au kupata maradhi ya akili.
Sehemu ya Sita: Ushuhuda wa Hakimu/Wakili

Kutokana na Mkataba wa Mkopo kuwa ni hati ya kisheria inayoziwajibisha pande mbili za mkataba, mkopaji anapaswa kujaza taarifa zake kwenye mkataba kwa kushuhudiwa na kuthibitishwa na hakimu au wakili. Ushuhuda wa Hakimu au Wakili utakubalika endapo kutakuwa na saini na muhuri wa Hakimu au Wakili husika. Ushuhuda wa Hakimu unaokubalika ni kuanzia Hakimu ya mahakama ya Wilaya. Mawakili wa Mahakama Kuu ndio pekee wanaokubaliwa kuwepo kwa ushuhuda wao.

Muda wa kuchukua na kurejesha Mikataba ya Mikopo

Waombaji wote wapya wanaoteuliwa kupata mikopo wanalazimika kujaza mikataba ya mikopo iliyotayarishwa na BMEJZ. Mchakato wa kujaza mikataba ya mkopo huanza mara baada ya kutangazwa kwa majina ya waombaji walioteuliwa kupata mikopo na kurejeshwa kwenye ofisi za BMEJZ baada ya kukamilika kujazwa. Kila muombaji anapaswa kuwa ameshachukua na kurejesha mkataba uliojazwa kikamilifu kwenye ofisi za BMEJZ ndani ya siku sitini (60) tokea tarehe yalipoanza kutangazwa majina ya waombaji wapya walioteuliwa kupata mikopo kwa kufuata utaratibu utakaopangwa na BMEJZ.

Kila mwanafunzi anayeendelea na masomo kwa kutumia mkopo unaotolewa na BMEJZ analazimika kujaza mkataba mpya kila unapoanza mwaka mpya wa masomo na kuurejesha BMEJZ baada ya kukamilika kwake kwa kufuata utaratibu uliowekwa. Wanafunzi wanaoendelea na masomo wanapaswa kuanza kuchukua Mikataba mipya baada ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo na kuwa wamesharejesha mikataba iliyokamilika kujazwa ndani ya siku 60 tokea kuanza kwa mwaka mpya wa masomo katika chuo husika.

Mkataba uliokamilika lazima uwe umejazwa vifungu vyote kama inavyostahiki na kuwepo kwa vivuli vya viambatisho vyote muhimu ambavyo lazima viwe vimethibitishwa na mahakama au wakili. Miongoni mwa vivuli vya viambatisho vinavyopaswa kuwemo katika mikataba ya waombaji wote ni pamoja na:

 • Cheti cha kuzaliwa.
 • Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na Mtanzania vya muombaji na wadhamini wake.
 • Vyeti na matokeo ya masomo “transcript”.
 • Matokeo ya mitihani ya muhula na mwisho wa mwaka kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo.
 • Barua ya udahili wa kujiunga na chuo.
 • Vitambulisho vya kazi au uwanachama wa mfuko wa jamii vya wadhamini.
 • Risiti ya malipo ya mkataba au ithibati nyengine yoyote ya malipo ambayo BMEJZ itaona inafaa.
 • Ithibati kutoka vyombo vya dola kuthibitisha kutojihusisha na uhalifu au makosa mengine ya jinai kwa mkopaji.

Aidha, mikataba itakayowasilishwa na wakopaji walioajiriwa inapaswa kujumuisha nyaraka za ziada zifuatazo:

 • Kivuli cha kitambulisho na uwanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii.
 • Kivuli cha kitambulisho cha kazi.
 • Barua ya ruhusa ya kuhudhuria mafunzo kutoka kwa mwajiri.
 • Ithibati ya malipo ya mshahara wa kila mwezi (salary slip).

Angalizo: BMEJZ inaweza kusitisha kutoa mkopo kwa mhusika endapo haitaridhika na taarifa zilizotolewa au mkopaji kukiuka masharti ya mkataba.

Muhtasari wa ratiba ya kazi ya BMEJZ kwa mwaka

Katika kutekeleza kazi zake kwa ufanisi, BMEJZ hufuata ratiba maalum ambayo kwayo huwa ni ukumbusho kwa watendaji wake na waombaji wapya na wanaoendelea na masomo wanaokusudia kuomba mikopo kwa mwaka mpya wa masomo. Ratiba kamili ya kazi ni kama ifuatavyo:

Na. Tarehe Kitendo Mhusika
1 Mei 02 hadi Julai 31 Utoaji wa Fomu za Maombi ya Mikopo kwa waombaji wapya Watendaji wa BMEJZ/waombaji wa mikopo
2 Agosti 01 hadi Agosti 31
 • Uingizaji wa taarifa za waombaji wapya wa mikopo kwenye database ya BMEJZ
 • Uhakiki wa waombaji waliotimiza sifa za msingi za kupatiwa mikopo.
 • Utayarishaji wa orodha za awali za waombaji wanaopendekezwa kwa uteuzi
Watendaji wa BMEJZ
3 Septemba 1 hadi Oktoba 31
 • Utoaji na urejeshaji wa Mikataba ya Mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo
 • Ulipaji wa ada Muhula wa kwanza na posho kwa Vyuo vya nje
Watendaji wa BMEJZ
4 Septemba 1 hadi Septemba 10. Vikao vya Kamati ya Uteuzi wa waombaji wapya watakaopatiwa mikopo. Wajumbe wa Kamati ya Uteuzi Watendaji wa BMEJZ
5 September15 hadi September 25 Vikao vya Bodi ya Wakurugenzi ya BMEJZ kupitia na kuridhia taarifa ya uteuzi ya Kamati ya Uteuzi
 • Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi
 • Watendaji wa BMEJZ
6 September 25 hadi September30 Kutangazwa majina ya awali ya waombaji walioteuliwa kupatiwa mikopo ya elimu ya juu. Mkurugenzi wa BMEJZ
7 Oktober 01 hadi Novemba 30 Utoaji na urejeshaji wa mikataba kwa wanafunzi wachelewaji ambapo watalipa ziada ya asilimia 100 ya gharama za usimamizi wa mikataba. Watendaji wa BMEJZ
8 Novemba 30 Kufungwa kwa zoezi la utoaji na urejeshaji wa mikataba kwa wanafunzi wanaoendela na masomo. Watendaji wa BMEJZ
9 Oktoba 01 hadi November 30 Utoaji na urejeshaji wa Mikataba ya Mikopo kwa waombaji wapya Watendaji wa BMEJZ
10 December 01 hadi December 31 Utoaji na urejeshaji wa mikataba kwa wanafunzi wapya wachelewaji ambapo watalipa ziada ya asilimia 100 ya gharama za usimamizi wa mikataba. Watendaji wa BMEJZ
11 Januari -March
 • Uhakiki wa wanafunzi Vyuoni-Tanzania
 • Malipo ya ada na posho muhula wa pili Vyuo vya nje.
Watendaji BMEJZ na Maafisa mikopo
12 Februari 01 Kufungwa kwa zoezi la utoaji na urejeshaji wa mikataba kwa wakopaji wapya Watendaji wa BMEJZ
13 Machi Malipo ya ada vyuoni Muhula wa Pili Watendaji wa BMEJZ
14 April-May Ufuatiliaji wa risiti za malipo na fomu za malipo zilizosainiwa na wanafunzi vyuoni Watendaji wa BMEJZ